Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) inapenda kufahamisha umma, Taasisi za Elimu ya Juu na Wadau wote wa Elimu ya juu ndani na nje ya nchi kuwa dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026 limefunguliwa kuanzia leo tarehe 15/7/2025. Dirisha hili litakuwa wazi hadi tarehe 10/8/2025.
UTARATIBU WA MAOMBI YA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2025/2026
Makundi ya Waombaji wa Udahili
Maombi ya udahili wa kujiunga na Shahada ya Kwanza yanahusu makundi matatu ya waombaji:
a) Wenye sifa stahiki za Kidato cha Sita;
b) Wenye sifa stahilki za Stashahada (Diploma), au sifa linganifu; na
c) Wenye sifa stahiki za Cheti cha Awali (Foundation Certificate) cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Ili kufahamu sifa stahiki kwa makundi matatu yaliyotajwa hapo juu, vyuo na programu zilizoruhusiwa kudahili, waombaji wanapaswa kusoma vigezo vilivyooneshwa katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyotolewa na TCU (Bachelor’s Degree Admission Guidebooks for 2025/2026 Academic Year) vinavyopatikana katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).