Mfano wa Barua ya Maombi ya kazi/Ajira kutoka UTUMISHI PSRS – Ajira Portal
Anna Mwakitalema,S.L.P. 456,
Kigoma,
28 Aprili 2025.
Katibu,
Ofisi ya Rais,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
S.L.P. 2320, Dodoma
YAH: MAOMBI YA KAZI YA UALIMU WA SHULE YA SEKONDARI
Ndugu Katibu,
Kwa heshima na taadhima, napenda kuwasilisha maombi yangu ya kazi ya Ualimu wa shule ya sekondari, kama ilivyotangazwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kupitia tangazo la ajira lililotolewa tarehe 20 Aprili 2025.
Nina Shahada ya Elimu (B.Ed.) ya masomo ya Kiswahili na Historia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, niliyoipata mwaka 2022. Nimepata uzoefu wa kufundisha kwa kipindi cha miaka miwili katika shule ya sekondari ya Serikali, ambapo nilionyesha uwezo mkubwa katika kufundisha, kuandaa zana za kufundishia na kujenga mahusiano bora na wanafunzi pamoja na walimu wenzangu.
Nina sifa, nidhamu, na uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa kufuata maadili ya taaluma ya ualimu. Naamini kuwa nikipewa nafasi hii nitatoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha taaluma kwa wanafunzi na shule kwa ujumla.
Naambatanisha nakala za vyeti vyangu vya taaluma, wasifu binafsi (CV), cheti cha kuzaliwa, pamoja na barua ya utambulisho kama sehemu ya nyaraka za kuunga mkono maombi yangu.
Natumaini barua yangu itapokelewa na kuzingatiwa. Nitashukuru sana kwa fursa ya kuitwa kwenye usaili ili kueleza kwa undani uwezo wangu.
Wako mwaminifu.
(Sahihi)
Anna Mwakitalema
Simu: 07XXXXXX
annamwakitalema@gmail.com